TUANZE 1
Mtaa ulifurika shamrashamra kwa sherehe nyumbani kwa Mzee Chombo. Ni binti yake Jamila ndiye alikuwa anaolewa siku hiyo. Watu wengi sana walifurika kwenye nyumba ya mzee huyo iliyokuwa na wapangaji saba. Watu walikula na kunywa huku matarumbeta yakisikika mtaa mzima na kuwagusa wapenzi wa hayo mambo.
Mauno ya kunengua kwa kundi la Baikoko Ilala yaliwakonga nyoyo za wanaume hasa vijana wa rika la sasa.
Hawakuwa na aibu hata kidogo kufunua nguo zako walizovaa sare na kuacha shanga na chupi za kizungu (bikini) zitazamwe na watu wote waliowakodolea macho eneo hilo.
Wale wenye kutamani walibaki kumeza mate tu huku wakiachia tabasamu kwa burudani wanayotoa Baikoko Ilala. Huku baadhi ya wamama wakiwageuze pembeni watoto wao wasishuhudie laana hiyo.
Siku hiyo ndio kijana Badu alikuwa njiani kwenye gari aina ya Center na dereva, gari lililobeba vitu vyake kwaajili ya kuhamia kwenye chumba chake kipya.
Alikuwa na furaha sana siku hiyo baada ya kutimiza lengo lake la kuhamia kwenye nyumba mpya anayofikia ambayo walikuwa wakikaribia kufika muda huo.
Akiwa kwenye furaha hiyo walisikia matarumbeta na shangwe zikisikika kwenye huo mtaa. Na jinsi wanavyozidi kusogea mbele ndio sauti hiyo inavyozidi kusikika.
“Ebwana eh! Ona nyomi hiyo kwenye hiyo nyumbo hapo mbele! Tutapita kweli hapo?”alisikika Dereva wa Center akipunguza mwendo akitembea taratibu.
” Dah aisee ishakuwa jau, na sikujua kama leo kuna sherehe hapa.”alisema Badu.
“Ah si tunatafuta njia nyengine tupite!”
“Bro hapo ndio tunafikia. Hiyo ndio nyumba yenyewe nayoingiza vitu hivi.”
“Hee kumbe ndio tunafikia hapa! Sasa itakuwaje mzee na unaona sherehe kama hivyo!”alihoji yule dereva akiamua kulipaki gari kwanza pembeni kwanza wakijadili.
“Dah hebu wacha nishuke nikacheki mazingira kwanza. Ikiwezekana niongee na mwenye nyumba.”
“Fanya hivyo mzee chombo inasubiriwa hii kubeba mzigo mwengine Mwenge.”
Alishuka Badu na taratibu akaanza kupiga hatua kusogea kwenye mkusanyiko wa sherehe. Wanawake walikuwa wamenogewa kwa utamu wa muziki na tarumbeta. Walizidi kucheza pale kati huku wakisasambua kila mtu akionesha ufundi wa kukata mauno.
Badu alipita kiubavu ubavu hadi kufikia geti la nyumba hiyo akapata kufungua kuingia ndani.
Huko alikutana na watu kadhaa wakipata chakula muda huo baada ya ndoa kufungwa. Alipiga macho huku na kule kutafuta mtu ambaye anamfahamu na kwa bahati alipata kuona sura ya msichana mmoja aliyemfahamu. Alipiga hatua hadi pale alipo na kupata kuonekana.
“Hee karibu kaka yangu, kwema?”alisikika msichana yule akiwa amejipodoa haswa.
“Kwema sista vipi naona mnasherehe hapa.”
“Ehe mwaya dadangu anaolewa leo ndio tunamalizia hapa.”
“Aisee sikujua mapema kama kuna sherehe leo. Ila sio kesi sema nini, leo ndio nimekuja na vitu vyangu vipo kwa nje kwenye gari nimekodisha. Sasa nimeona hapa nje nyomi ya watu nimeshindwa kuleta gari mpaka hapo. Sasa sijui nafanyaje na mwenyewe anataka kuondoka.”aliongea Badu akiwa anamtazama binti yule aliyejulikana kwa jina la Mwajuma.
“Oh jaman pole mwaya, hebu ngoja kwanza nikaongee na mama tujue tunafanyaje. Naomba nisubiri hapa. Umekula kwanza?”
“Ah wala usijali hapa kwanza nataka nishushe vitu maswala ya kula hata baadae.”
“Sawa nisubiri dakika sifuri.”aliongea Mwajuma na kugeuka kuondoka zake.
Badu akabaki kumtazama tu msichana huyo akiyejaaliwa maungo yake nyuma.
Alijikuta anazuia matamanio yake hayo ya gafla kwenye mji wake mpya huo.
Alisogea pembeni kuketi kwanza huku akitazama chumba chake kilichopo karibu pembeni yake wamekaa nje wamama wakiwa hawana habari wanakula.
“Dah leo mbona jau sana! Watu wote hawa nitaingizaje vitu humu.”alijisemea mwenyewe bila ya kupata jibu kamili. Punde tu simu yake iliita na kuona ni yule dereva wa gari anapiga, ikabidi apokee.
“Ndio bro.”
“Dogo vipi mbona kimya?”
“Bro ndio naongea na mwenyewe hapa tujue tunafanyaje.”
“Fasta basi si unajua nina kazi nyengine.”
“Usijali kaka tunaweka mambo sawa.”aliongea Badu na simu ikakatwa.
Alishusha pumzi asijue nini kitajiri.
“Shoga hiki chumba yule ostadhi amehama kumbe?”
“Eh we wawapi! Mbona kaondoka anasiku ya tano sasa, nilisikia za chinichini mama J alikuwa anamlazimisha kila siku atembee naye lakini Ostadh anaimani ya kweli. Kaona isiwe shida kaondoka hata miezi mitatu hajamaliza na kodi yake kaisamehe.”
“Mh huyu mama naye hana aibu, kila mpangaji anataka amkaribishe yeye.”
“Utamuweza huyo, na ndio mama mwenye nyumba wetu tutafanyaje.”
Yalisikia mazungumzo hayo ya wanawake wakiwa wamekaa kwenye chumba ambacho Badu alipaswa kuhamia hapo. Maongezi hayo aliyasikia vema na kubaki kuwatazama tu asijue kinachomaanishwa.
Muda huohuo Mwajuma alirudi akiwa na mama yake moja kwa moja hadi pale alipo Badu, huku watu wakimwita Mama huyo na kumshangilia kama mama shuhuli.
“Oh karibu baba. Hujambo.”alisalimia mama huyo ambaye ndiye mwenye nyumba, Mama Jamila.
Badu alibaki kumtazama mama huyo ambaye sekunde chache tu ametoka kusikia wanawake pembeni kuhusu taarifa za mama huyo.
ITAENDELEA.
All Rights Reserved © | Simulizi TAMU