NILIMPENDA KUPITA KIASI (07)

Sehemu ya 7:

“Ukweli Unaacha Alama” 

Simulizi ya kweli – kama inavyosimuliwa na Tunu

Sikuweza kulala. Kila nikiweka kichwa changu kwenye mto, mawazo yalikuwa yanazunguka kichwani mwangu kama upepo wa baharini unaovuma bila utulivu.
Nilihisi kuna kitu hakiko sawa, lakini nilikuwa naogopa kujua ukweli.
Unajua ile hali ya kujua kitu kinakuumiza, lakini bado hutaki kuthibitisha kwa sababu unaogopa kukipoteza? Ndivyo nilivyokuwa.

Siku moja nilimwambia Brian,

“Nataka tukae tuzungumze vizuri. Najisikia vibaya siku hizi.”

Alinikwepa.

“Tunu, si nilikuambia kazi zimenichosha sana? Tutazungumza weekend, sawa?”

Weekend ilifika, lakini hakutokea. Nilimpigia simu mara nne — hakupokea. Nilimtumia ujumbe mfupi:

“Uko salama?”

Hakujibu.
Nilijisikia dhaifu, nikaamua kwenda kwake moja kwa moja. Nilijua anapoishi — nilishawahi kufika pale mara moja aliponiambia nimtembelee.

Nilipofika, moyo wangu ulikuwa unadunda kwa nguvu. Nilijisemea, labda nimemkosea, labda ananiavoid kwa hasira.
Lakini nilichokiona pale kilibadilisha kila kitu.

Nilipofika nje ya geti, niliona gari lake limeegeshwa — lile lile ninalolijua vizuri. Nilihisi furaha kidogo, nikafikiri, “Ah, kumbe yuko nyumbani!”
Nilikaribia mlangoni, nikataka kugonga.
Lakini kabla sijagonga, mlango ulifunguliwa kutoka ndani.

Nilisikia sauti ya mwanamke ikicheka, kisha Brian akasema kwa upole,

“Mpenzi, subiri nikupeleke hadi chini kidogo.”

Nilisikia sauti hiyo ikiendelea, ikiunguruma ndani ya moyo wangu kama radi.
Mwanamke alitoka akiwa amevalia t-shirt yake Brian — ile niliyonunua siku ya Valentine.

Nilihisi miguu yangu ikitetemeka. Nilijificha nyuma ya ukuta, nikimuona akimfungulia mlango, wakatoka wakicheka.
Macho yangu yalijaa machozi. Nilishindwa hata kupumua.

Nilihisi dunia ikinisaliti.
Nilitaka kutoka nimkabiliane, nimwambie, “Mbona umenidanganya?” Lakini neno halikutoka. Nilihisi udhaifu wa ajabu.
Niliangalia tu, nikimuona akimshika mkono yule mwanamke, wakiondoka kwa furaha.

Nilikaa pale kwa dakika kadhaa, nikilia kimya kimya.
Niliwaza zile meseji, zile ahadi, yale maneno yake matamu… na nikajua, yote yalikuwa uongo.

Usiku ule nilirudi nyumbani nikiwa nimevunjika vipande vipande.
Nilijaribu kumtumia meseji, lakini hakujibu.
Nilijua amechagua kimya chake kama kisu cha kunikata polepole.

Nililala nikilia, nikisema kwa sauti ndogo,

“Nilimpenda kupita kiasi… na labda hicho ndicho kilikuwa kosa langu.”

Siku iliyofuata, nilipokea meseji moja tu kutoka kwake:

“Tunu, naomba unisamehe. Nitakueleza kila kitu, lakini si sasa.”

Niliisoma mara kumi. Kila herufi ilinikata moyo.
Nilijua majibu yatakuja — lakini nilijiuliza, je, nitakuwa tayari kuyasikia?

 Ukweli unauma zaidi pale unapotoka kwa mtu uliyemuamini kupita dunia nzima.

 Itaendelea…

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Share kwa ndugu na marafiki

WhatsApp
Facebook
X

Chagua kipande kinachofuata