NILIMPENDA KUPITA KIASI (15)

Sehemu ya 15:

Miezi mitatu ilipita tangu mimi na Kevin tuanze rasmi uhusiano wetu.
Haikuwa kwa haraka, haikuwa kwa presha  ilikuwa safari ya utulivu, ya kuheshimiana.
Tulijifunza kila siku kitu kipya kuhusu sisi.

Nilipenda jinsi alivyokuwa makini, jinsi alivyoheshimu muda wangu na kazi yangu.
Na zaidi ya yote, nilipenda namna tulivyoweza kuzungumza kila kitu bila hofu.
Tulikuwa marafiki kabla ya kuwa wapenzi  na hilo lilifanya kila kitu kuwa rahisi.

Lakini kadri siku zilivyopita, nilianza kugundua jambo.
Kevin alikuwa na changamoto kwenye biashara yake.
Mauzo ya duka lake la viatu yalikuwa yanashuka, na mara nyingi nilimuona akiwa na mawazo.

Nilijaribu kumtia moyo, lakini siku moja alinijibu kwa hasira, kitu ambacho hakuwahi kufanya.

“Tunu, si kila kitu kinaweza kutatuliwa kwa maneno mazuri! Hii siyo semina ya wanawake wako, hii ni maisha halisi!”

Nilinyamaza.
Siku taka kujibizana, ila maneno yake yaliniuma kidogo.
Lakini nilijua, wakati mwingine mtu akiumia, anaweza kuongea kwa uchungu.

Siku iliyofuata alinipigia simu akisema,

“Samahani sana, Tunu. Nilikuwa nimekasirika, si kwa sababu yako, bali kwa hali yangu. Sikuwezi kukosea heshima.”

Nilimjibu kwa upole,

“Sawa, Kevin. Nimekuelewa.
Lakini kumbuka, upendo si maneno matamu tu ni uvumilivu na uelewa.”

Tulimaliza mazungumzo kwa amani, lakini moyoni nilijua  hii ndiyo hatua ambayo mapenzi ya kweli yanapimwa.

Miezi miwili baadaye, mambo yalizidi kuwa magumu.
Kevin alianza kujitenga kidogo, labda kutokana na presha ya biashara.
Nilijaribu kumkaribia, lakini nilihisi kama anazama kwenye kimya chake mwenyewe.

Siku moja nilimtembelea bila kumwambia. Nilimkuta duka liko wazi, lakini ndani hakuwa yeye.
Nilikaa nje dakika chache, nikijaribu kumsubiri.
Baada ya muda, nilimuona akija akiwa amechoka  lakini si tu mwilini, bali moyoni pia.

Alinipomwona, macho yake yalijaa hisia.

“Tunu,” alisema kwa sauti ya chini, “nimechoka. Wakati mwingine najihisi kama siwezi tena.”

Nilimsogelea, nikashika mikono yake, nikasema kwa utulivu,

“Kevin, hata nilipokuwa nimevunjika, Mungu aliniacha niishi.
Hivyo na wewe, hupaswi kukata tamaa. Tuko pamoja.”

Alinitazama, macho yake yakianza kububujika machozi.

“Ndio maana nilikuomba uwe karibu nami  kwa sababu unanifanya niamini tena.”

Tulikumbatiana kimya kimya katikati ya duka lake dogo, likiwa tupu lakini likijaa upendo wa kweli.
Siku hiyo nilijua  hatima haikuwa tu kukutana, bali kusaidiana kusimama.

Upendo wa kweli haukimbii dhoruba  unashika mkono wako na kukuvusha salama upande wa pili.

 Itaendelea…

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Share kwa ndugu na marafiki

WhatsApp
Facebook
X

Chagua kipande kinachofuata