
NILIMPENDA KUPITA KIASI (19)

Sehemu ya 19:
Nilikuwa nimekaa kwenye mgahawa mdogo wa mjini, ule niliupenda kwa sababu ya utulivu wake na kahawa ya tangawizi yenye harufu ya kupendeza.
Nilikuwa na laptop yangu, nikiandaa ripoti ya kazi, wakati nikasikia sauti ya kiume ikisema kwa upole:
“Samahani dada, naweza kaa hapa? Meza zote zimejaa.”
Nilinyanyua macho na hapo ndipo nilimwona Brian kwa mara ya kwanza.
Alikuwa amevaa shati jeupe safi na suruali ya bluu ya kawaida, tabasamu lake lilikuwa la adabu.
Nilimruhusu akae.
Tulikaa kimya kwa dakika kadhaa, kila mmoja akiwa bize na kazi yake, mpaka aliponiambia,
“Unaandika vizuri sana. Nilikuwa naona namna unavyotazama screen kama mtu anayeishi kwenye hadithi.”
Nilicheka kidogo.
“Labda kwa sababu kweli mimi ninaishi kwenye hadithi, Brian,” nilijibu bila hata kujua nimemtaja jina.
Akanitazama kwa mshangao, akacheka.
“Sasa umejuaje jina langu?”
Nikagundua jina lake lilikuwa limeandikwa kwenye kitambulisho kilichoning’inia kifuani mwake.
Tukaendelea kucheka kwa upole na hapo mazungumzo yakaanza.
Tulizungumza kwa muda mrefu kuliko nilivyotarajia.
Alikuwa mcheshi, mchangamfu, lakini zaidi ya yote alikuwa msikivu.
Hakuharakisha kuuliza maswali ya faragha, wala kuonyesha haraka hisia.
Alionekana kama mtu anayeheshimu mipaka ya mwingine, jambo ambalo lilinigusa sana.
Baada ya saa moja, alisimama kuondoka, akaniambia,
“Nilifurahia sana kukutana nawe, Tunu. Natumai siyo mara ya mwisho.”
Nilitabasamu, nikajibu,
“Maisha yana njia zake. Kama ni mpango wa Mungu, tutaonana tena.”
Na kweli, siku haikupita nyingi kabla hatujakutana tena safari hii, kwa bahati, kwenye kikao cha kazi cha mashirika mawili tofauti tuliyokuwa tunashirikiana.
Tulitabasamiana tu, lakini ndani yangu, nilihisi kitu cha kipekee.
Siyo kama hisia za haraka au tamaa ilikuwa ni amani.
Tangu siku hiyo, tulianza kuwasiliana mara moja moja.
Hakuwahi kunisukuma, hakuwahi kuniuliza maswali mengi.
Alijua nimepitia machungu, na kila neno alilosema liliheshimu safari yangu.
Na mara nyingi nilijiuliza kimoyomoyo:
“Labda huu ndio mwanzo wa hadithi mpya, lakini safari hii nikiwa nimepona.”
Wakati mwingine Mungu hatuletei mtu kutufurahisha, bali kutuonyesha kwamba bado tunaweza kutabasamu tena.
Itaendelea…

