
NILIMPENDA KUPITA KIASI (44)

Sehemu ya 44:
Siku ya safari ya kwenda London ilifika haraka kuliko nilivyotarajia.
Nilikuwa nimeshinda usiku mzima nikiwaza sio kwa hofu, bali kwa msisimko.
Mawazo yaliruka kama vipepeo:
Je, nitashinda tuzo?
Je, hotuba yangu itawagusa kama ile ya Cape Town?
Je, nitaweza kuiwakilisha Afrika vizuri?
Lakini kila mara nilipohisi presha, nilimtazama Amani na moyo wangu ukatulia.
Alikuwa ndiye mwanzo wa safari yangu mpya, na sasa alikuwa sehemu ya kila hatua.
Safari Ya Kwanza Ya Amani Ndege Kubwa
Uwanja wa ndege ulikuwa na pilika pilika nyingi.
Amani alinishika mkono kwa nguvu, macho yake makubwa yakiangalia kila upande kama mtoto aliyeingia sokoni kwa mara ya kwanza.
“Mama hii ni nyumba inaruka?”
Aliuliza na sauti yake ya utundu.
Nilicheka, nikainama kumkumbatia.
“Hii inaitwa ndege, mwanangu.
Itatupeleka mbali mbali sana.”
Asha aliwahi kutupeleka mpaka getini. Alinibusu shavuni, akamshika Amani akamwambia:
“Ukifika huko Ulaya, mwambie dunia ijue mama yako ni shujaa.”
Niliona macho ya Asha yakigota machozi lakini akajitahidi kuyazuia.
Safari hii haikuwa ya kawaida ilikuwa mwanzo wa ukubwa.
🌧️ London Hewa Baridi ya Neema
Tulipoteremka London Heathrow, hewa baridi ilinigusa usoni kama upepo wa barafu wenye harufu ya mvua.
Nilimfungia vizuri Amani koti lake jekundu, naye akalia kidogo kwa baridi.
Mwanaume wa shirika lililonialika alisimama na bango lililoandikwa:
“WELCOME TUNU GLOBAL WOMEN WRITERS AWARDS.”
Nilipomsogelea, uso wake ulijaa mshangao safi.
“You look younger than I expected,”
akasema akicheka.
“Your story… it has traveled farther than you know.”
Maneno yake yalinipenya rohoni.
Je, kweli sauti yangu imefika mbali kiasi hicho?
Hoteli Ya Ndoto – The Royal Crescent
Walitupangia hoteli ya kifahari ukumbi mkubwa wenye chandeliers za dhahabu, mazulia laini chini ya miguu, na dirisha lililoangalia mto Thames.
Nilisimama kimya kwa muda, nikishika pazia kwa taratibu.
“Mama, hapa tutaishi?”
Amani aliuliza kwa mshangao.
“Ndiyo mwanangu… lakini ni kwa siku chache tu.”
Nilimtazama, nikafumba macho kwa sekunde chache.
Yule Tunu wa miaka iliyopita aliyewahi kulia gizani, aliyewahi kudharauliwa, aliyewahi kutetemeka kwa maumivu—huyu hapa leo, anasimama kwenye hoteli ya kifahari jijini London.
Mungu ni mwandishi wa hadithi isiyotarajiwa.
Mazungumzo Na Waandishi Wakubwa
Kesho yake, kulikuwa na mkutano wa waandishi waliongia kwenye shortlist.
Nilikaa meza moja na wanawake kutoka mataifa tofauti India, Canada, Brazil, Ethiopia, Korea.
Mmoja wao, mwandishi maarufu kutoka Canada, aliniangalia kwa makini akasema:
“Tunu, your book is pure courage.
How did you survive everything you wrote?”
Nilitabasamu taratibu, nikajibu kwa sauti ya utulivu ambayo hata mimi sikuijua:
“Nilijifunza kitu kimoja…
Ukichagua kuishi, dunia itafunguka kwa namna yake.”
Walinitazama kimya kimya cha heshima.
Kile kimya kilinipa ujasiri kuliko makofi.
🎤 Siku Ya Tuzo Ukumbi Uliojaa Historia
Ilipofika siku ya tuzo, walinipa gauni jeupe jeupe lililokuwa na mkia mrefu na shanga ndogo kama nyota.
Nilipolivaa, nilijitazama kwenye kioo nikamuona mwanamke mpya.
Mwanamke aliyepitia jivu na akafufuka kama pembe ya moto mpya.
Ukumbi ulikuwa mkubwa, wenye mwanga mkali na camera nyingi.
Nilipofanya kazi ya kuingia, watu walisimama sio kwa kelele, bali kwa heshima tulivu.
Niliketi kwenye kiti cha mbele, Amani akiwa ameshikwa na mhudumu maalum.
Alikuwa akinitazama kwa macho ya fahari.
Moyo wangu ulikuwa ukipiga kama ngoma za asili za Kilwa.
Kisha…
Mshereheshaji akapanda jukwaani.
Akasema:
“And the winner of the Global Women Writers Award 2026 is…”
Ukumbi wote ukawa kimya.
Nilihisi damu ikipanda kichwani.
“…TUNU MWAKALE Healing Through Loss.”
Ukumbi mzima ulilipuka kwa makofi.
Nilishtuka.
Nilishindwa kusimama.
Machoni pangu palifunikwa na machozi.
Niliinuka taratibu…
Nikaenda jukwaani…
Nikasimama mbele ya dunia…
Na nikasema:
“Sauti ya mwanamke aliyewahi kuumia
inaweza kuangaza dunia nzima.
Mimi ni ushahidi.”
Watu walisimama, wakapiga makofi kwa muda mrefu.
Amani alikimbia jukwaani akanikumbatia kiunoni.
Ukumbi ukaongezeka kelele za furaha.

