
NILIMPENDA KUPITA KIASI (50) MWISHO

SEHEMU YA 50 (MWISHO
Siku ile…
Siku ambayo yote ilipaswa kuisha kwa giza, ndipo niligundua kuwa wakati mwingine Mungu hukaa kimya kwa muda mrefu ili mwisho akija akiongee, ujumbe wake uwe wazi zaidi.
Baada ya siku ile ya vurugu na mshtuko, niliamka hospitalini nikihisi mwili mlegevu lakini moyo ukiwa mwepesi. Kukaa kitandani pale, nikitazama dari jeupe, kulikuwa na utulivu mwingi kuliko nilivyowahi kuwa nao kwa muda mrefu.
Brian alikuwepo pembeni yangu, akilale kwenye kiti, kichwa kikiwa kimeegemea ukingo wa kitanda changu. Nilimuangalia kwa muda mrefu… kwa utulivu.
Kwa upendo.
Kwa shukrani.
Nilimgusa kidogo mkono. Akastuka, akaniangalia, macho yakiwa mekundu kama mtu aliyelia kwa muda mrefu.
“Tunu… Mungu ni mwema,” aliniambia kwa sauti ya upole.
Nikacheka kidogo. “Ndiyo, ni mwema kuliko tulivyowahi kufikiria.”
Kulikuwa na utulivu ule ambao huja baada ya vita kubwa kukoma utulivu wa mtu aliyepigana, ameumia, lakini bado yuko hai.
Siku zilizofuata zilikuwa safari ya kujiponya. Sio tu mwili, bali moyo.
Nilikaa nikitafakari maisha yangu… jinsi nilivyopoteza, jinsi nilivyojaribu kusimama, jinsi nilivyovunjwa tena, na vile nilivyoamua kupigania amani yangu.
Nilipata muda wa kujielewa.
Nilijifunza kuwa kuumia hakunifanyi dhaifu.
Kilichonifanya kuwa dhaifu ni kukubali kuendelea kuishi ndani ya maumivu baada ya muda wake kwisha.
Siku moja kabla sijatoka hospitali, mama yangu alinipigia simu. Sauti yake ilikuwa ya utulivu uliokomaa.
“Tunu mtoto wangu… maisha yamekufundisha mengi. Lakini nataka ujue kitu kimoja… hujazaliwa kuumia. Umezaliwa kupenda na kupendwa kwa heshima. Usirudi kwenye kivuli ambacho Mungu amekutoa.”
Nilitulia kimya kwa sekunde kadhaa. Kisha nikasema:
“Mama, safari hii siwezi rudi nyuma. Nimeiona thamani yangu.”
Na kweli, niliiona.
Nilipotoka hospitali, ulimwengu ulionekana tofauti.
Baridi ya asubuhi ilikuwa tamu.
Mwanga wa jua ulionekana mpya.
Na ndani yangu kulikuwa na amani ambayo sikuielewa mwanzoni hadi baadaye nilipojua:
Ilikuwa ni amani ya kujikubali.
Amani ya kuacha yaliyopita yasinitawale.
Amani ya kufahamu kwamba moyo wangu umepitia mengi, lakini haujafa.
Siku ya mwisho nilipomuaga Brian kabla ya kurudi nyumbani, nilimshika mkono na kumwambia:
“Asante kwa kuwa sehemu ya safari yangu. Sijui kesho inashikilia nini, lakini leo… leo niko salama.”
Alinitazama kwa macho yenye upole mwingi na kusema:
“Tunu… hauhitaji kunilipa kwa wema. Wema hauhitaji malipo. Unachohitaji ni kuishi. Kuishi vizuri. Kuishi bila hofu.”
Nilitabasamu.
Tulifungiana mikono kwa muda mfupi, kisha tukatengana kwa utulivu wa watu wanaojua kuwa hatima haipitwi kwa nguvu bali kwa wakati.
Nilipofika nyumbani, niliingia chumbani kwangu, nikaangalia kioo.
Niliona mtu mpya.
Mtu ambaye aliteseka lakini bado anasimama.
Mtu aliyependa kupita kiasi, akavunjika kupita kiasi, akajiponya kwa juhudi zake.
Nikaandika maneno haya kwenye diary yangu, ambayo nitayahifadhi kama ushuhuda wa maisha yangu:
“Sikuchagua kupenda vibaya. Lakini nimechagua kuponya vizuri.”
Na hapo simulizi yangu ilikamilika si kwa kishindo, si kwa kilio, si kwa faraja ya mapenzi mapya bali kwa ushindi wa ndani.
Ushindi ambao kila mtu ambaye amewahi kuumia anaweza kuufikia.
MWISHO


One Comment
but hujatuambia uliamua kuwa na nani au kumchagua nani na mtu aliekuja usiku kwako kwako ni nani vipi kuhusu mtoto na kelvin na Brian